SUNDAY MANARA AKA COMPUTER
FAHARI YA WANAKIGOMA
Huyo bwana anaitwa
SUNDAY RAMADHANI MANARA aka ‘Computer’ aliyezaliwa miaka 54 iliyopita mjini
Kigoma mahali ambapo palikuja kuwa chimbuko la wachezaji wengi nyota kama akina
Hamis Askari, Aloo Mwitu, Athuman Juma, Juma Kampala, Abeid Mziba, Makumbi Juma
na wengineo.
Mkongwe huyo, ambaye ndugu zake wawili nao walikuwa wanapiga soka yaani Kitwana
Manara kaka yake na mdogo wake Kasimu Manara kwa sasa anapatikana maeneo ya
Temeke, jijini Dar es Salaam.
MAISHA YA UTOTONI KATIKA
SOKA
Sunday anakumbuka maisha
yake ya utotoni alianza kuchezea Young Kinya ambayo ilikuwa kama timu ya watoto
wa Yanga ingawa ilikuwa kama inajitegemea zaidi na ilikuwa inafanya mazoezi nje
ya viwanja vya Kaunda na ilikuwa ukitoka pale unasogea kidogo unakwenda Afrikan
Boys ambayo ilikuwa ni timu ya pili ya Yanga na mwanzoni mwa miaka ya 1970
Sunday na wenzie akina Awadhi Kessy, Douglas, Shabaan Ufunguo, Mohamedy Ugando
walipandishwa kuichezea Yanga ya wakubwa chini ya kocha Profesa Victor
Stanculescu na huko waliwakuta kina Elias Michael, Mohammed Msomali, Hassan
Goboss, Boi Iddy, Athuman Kilambo, Maulidi Dilunga, Badi Salehe, Leonard
Chitete na wengineo.
MALEZI YAKE KWA
STANCULESCU
Sunday, ambaye binafsi
anakiri kuwa hajui jina la mashine hiyo yenye kufanya kazi vizuri alipewa na
nani zaidi ya kukumbuka tu ni mwaka 1975 alipotoka Zanzibar baada ya kuwapiga
Simba mabao 2-0 ila anakubali kuwa maisha waliyokuwa wanalelewa na Mzungu huyo
yalimfanya aipende sana Yanga kuliko timu nyingine yeyote ikiwamo Taifa Stars,
ambayo walikuwa wachezaji takribani saba, ambao ni kipa Elia Michael, Athuman
Kilambo, Hassan Gobboss, Abdulhaman Juma, Kitwana Manara, Gibson Sembuli na
yeye mwenyewe.
Ushirikiano ulikuwa mkubwa na ulisababisha kuwa mara zote ni furaha tupu ndani
ya mitaa ile ya Jangwani hadi mwaka 1973 ambapo Simba ilifuta uteja kwa
kuwafunga bao 1-0 lililowekwa kimiani na nahodha wa Simba wakati huo, Haidar
Abeid Muchacho
SUNDAY MANARA NA SIMBA
Sunday anasema mara zote alizokuwa akikutana na Simba alikuwa anawaua tu bila
masihara, mwaka 1971 Simba ilifungwa mabao 2-0 na moja alifunga yeye na jingine
alifunga Maulid Dilunga, mwaka 1974 mechi ya kihistoria ambayo ilipigwa mjini
Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana, Simba ilifungwa mabao 2-1, yaliyofungwa na
Adam Sabu kwa upande wa Simba kabla ya Gibson Sembuli kufunga dakika ya 87 na
Sunday Manara kushindilia msumali wa mwisho dakika 30 za nyongeza.
Mechi nyingine ilikuwa ni fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki iliyopigwa
mjini Zanzibar katika Uwanja wa Amaan na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0,
huku goli la kwanza likifungwa na Sunday Manara la umbali wa zaidi ya mita 25
na kusababisha utata mkubwa kwa manazi wa Simba wakimtuhumu kipa wao Athuman
Mambosasa kuwa aliachia makusudi au alipewa kitu kidogo na bao la pili
lilifungwa na Gibson Sembuli kama kawaida yake kwa shuti kali sana.
Mbali na kuifunga Simba mara zote hizo, Sunday pia alikuwa ni rafiki mkubwa
sana wa kipenzi cha Simba, Abdallah King Kibaden Mputa ambaye kwa sasa ni
meneja wa Simba.
Sunday pia alioa binti wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, mzee Hassan Haji
ambaye ni baba mkubwa wa Mohammed Mkweche aliyekuwa beki maarufu wa Pan
African.
Simba pia ndio waliofanikisha mpango mzima wa Sunday Manara kwenda kucheza soka
la kulipwa nje ili atoe balaa la wenyewe kufungwa na mtu huyo, huo ndio
uhusiano wake na Simba maarufu kama Lunyasi
KUVUNJIKA KWA YANGA
KUZALIWA PAN
Sunday akizungumza kwa masikitiko makubwa na bila kumungunya maneno anamtupia
lawama kubwa kocha raia wa Zaire wakati huo, Tambwe Leya kuwa baada ya kutolewa
na Enugu Rangers ya Nigeria katika mashindano ya Afrika aliwatuhumu wachezaji
nyota akina Sunday, Omary Kapera, Sembuli na wengineo kuwa wameihujumu timu
hadi kusababisha kufungwa hivyo wanachama kwa hasira wakawafukuza viongozi wote
wakiongozwa na mzee Tabu Mangara na Shiraz Sharif na kuwekwa viongozi wengine
ambao waliwataka wakiri makosa.Kwa kuwa hatukujua kosa letu, tukaondoka na
kuelekea Nyota Afrika ya Morogoro na baadaye tukarudi Dar es Salaam na kuunda
timu inaitwa Pan mwaka 1976, anasema.
SUNDAY MANARA NA SOKA LA
KULIPWA
Mwaka 1977 Sunday
alitimkia Uholanzi kupiga soka la kulipwa na alikuwa mchezaji wa kwanza
Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kwenda kucheza katika ligi kubwa Ulaya
katika timu ya Heracles ambayo ipo hadi sasa katika ligi hiyo na huko alikutana
na watu kama akina Jaan Rep, Ruud Krol, Johan Neeskens, Johan Cruyff ,Van
Hangem na wengineo. Alikaa huko mpaka mwaka 1979 alipotimkia nchini Marekani
ambako walikuwa wameanza mipango ya kukuza soka nchini kwao.
TENGA KAJIFUNGIA NA
FIKRA ZAKE
Sunday akizungumzia soka
la Tanzania anamshushia lawama nzito Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) Leodegar Tenga kuwa analipeleka soka kuzimu na kuwa hahitaji ushauri kwa
watu ambao anajua kabisa kuwa wamecheza soka kwa upeo mkubwa na soka
wanalielewa kama yeye.
Tenga hapendi kukosolewa
sasa mawazo mapya atayapata wapi? Namshauri kama mdogo wangu aitishe mdahalo wa
kitaifa tuzungumzie soka, tupo tunaojua matatizo ya soka si hao wenye vyeti na
soka hawalijui, anasema Computer ambaye kwa sasa yuko mbioni kuwa na Academy
yake ambayo itakuwa mfano wa kuigwa nchini
SOKA LA ZAMANI NA SASA
Computer anasema
viongozi wa zamani walikuwa na mapenzi makubwa na viongozi wenzao wa timu
nyingine na wachezaji wa upande mwingine pia wachezaji walikuwa wanapendana nje
ya uwanja, upinzani ilikuwa ndani ya uwanja.
Sunday, ambaye ni mpenzi
wa Barcelona ya Hispania anawasifia wachezaji kama Mbwana Bushiri, Emil Kondo
na John Lyimo kuwa walikuwa na vipaji vya hali ya juu, ingawa anakiri kuwa hata
sasa wapo wenye vipaji lakini wameshindwa kuvumbuliwa.